Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Machi 15, 2022 amemuapisha aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi pamoja na Waziri Kidamba kuwa mkuu wa mkoa wa Njombe.
Halfa ya kuwaapisha Polepole na Kidamba imefanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali.
Akizungumza baada ya kuwaapisha Viongozi hao Rais Samia amesema atakutana na Balozi Polepole na kuzungumza naye kirefu kabla hajaelekea nchini Malawi.
“Mheshimiwa Balozi Polepole najua baada ya hapa watakuweka darasani kwanza pale Chuo cha Diplomasia utakapotoka pale kabla hujaenda Malawi nitakutana na wewe, kwa hiyo tutazungumza kwa kirefu,” Amesema Rais Samia.
Kwa upande wa Kindamba ambaye ameapishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Njombe amemtaka kwenda kuangalia suala la lishe pamoja na kuhamasisha chanjo ya UVIKO – 19 katika mkoa huo.
“Mkuu wa Mkoa (Waziri Kindamba) unakwenda Njombe, ni mkoa wenye kila kitu kwa hiyo kama utatulia unaweza ukapandisha kipato kwa kiasi kikubwa pale Njombe lakini kuna mambo mengi ya kuangalia, pamoja na kuwa Njombe ni Mkoa unazalisha chakula kwa wingi sana lakini kuna tatizo la nutrition, kalitazame hilo,” Amesema Rais Samia.
Kabla ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Polepole alikuwa Mbunge wa kuteuliwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kidamba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).