Mshambuliaji kutoka Uganda na klabu ya Kagera Sugar Hamis Kiiza ‘Diego’ amesema kwa sasa wana wakati mgumu wa kupambana katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kufuatia mabeki wa timu pinzani kumkamia.

Mshambuliaji huyo aliyewahi kuzitumikia klabu nguli za Tanzania Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti kabla ya kurejea nchini kwao Uganda, alisajiliwa na Kagera Sugar wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu huu 2021/22.

Kiiza amesema tangu amefanikiwa kuifunga Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu uliounguruma Uwanja wa Kaitaba mwezi Januari, amekua akikamiwa na mabeki wa timu pinzani, huku akikiri kuwa ligi msimu huu ni ngumu.

Amesema naamini kiwango alichokionesha wakati wa mchezo dhidi ya Simba SC kimewashtua wachezaji wengine wanaocheza nafasi ya ulinzi katika timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, na wamedhamiria kumbana vilivyo ili asiwaletee madhara.

“Tangu niwafunge Simba wapinzani wananikamia, lakini wanasahau Uwepo wangu kwenye kikosi sio kigezo cha kufanya kila kitu, nisipofunga kuna mwingine atafunga hivyo kikubwa mchango wangu uonekane na sio kukamilisha tu idadi ya namba ya wachezaji.” amesema Kiiza

Usajili wa Kiiza ndani ya Kikosi cha Kagera Sugar kwa asilimia kadhaa umeleta tija kwa Kocha Mkuu Francis Baraza, ambaye amejua kumtumia kwa uzoefu wake, hali ambayo imepelekea timu hiyo kuwa na muendelezo mzuri katika ushindani wa Ligi Kuu.

Kim Poulsen awatema Bocco, Nyoni Taifa Stars
Nitanzungumza na Polepole kwa Kirefu-Rais Samia