Kiungo na NahodhaMsaidizi wa Young Africans Haruna Niyonzima amewataka wachezaji wenzake kukubali Presha iliopo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni.
Niyonzima amesema kama kuna mchezaji yoyote ndani ya Young Africans hataki kukubali Presha zilizopo katika timu yao, basi aache kucheza kabisa mpira kwa kuwa presha ni sehemu ya mchezo.
Amesema Presha ni sehemu ya mchezo wa soka, hivyo hawana budi kukubaliana na hali hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho Young Africans inafukuziwa kwa ukaribu na Simba SC na Azam FC kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Presha ni sehemu ya mchezo lakini mimi hainisumbui kabisa, sasa nitashangaa kuona mchezaji hakubali presha akiwa hivyo inabidi aache kabisa kucheza mpira,” amesema Niyonzima na kuongeza kuwa
“Young Africans kukosa ubingwa misimu mitatu mfululizo ndio sababu kubwa inayozidisha presha ndani ya timu na mimi hii ni mara ya kwanza kuwaona Yanga wakikosa kombe mara tatu mfululizo,” amesema Niyonzima.
Young Africans leo watashuka dimbani kucheza dhidi ya Gwambina FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kusaka alama tatu muhimu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.
Young Africans iliyocheza michezo 25 inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 54, huku Gwambina FC ikiwa kwenye nafasi ya 12 kwa kumiliki alama 30, zilizotokana na michezo 24.
Simba SC ambayo tayari imshacheza michezo 22, inashika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 52, huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 50, baada ya kushuka dimbani mara 26.