Jeshi la Polisi Mkoani Kagera limemkamata Paschal Kaigwa Mariseli (21) mkazi wa mtaa wa National housing kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba mtuhumiwa wa ya mauaji ya Hadija Ismail (29) baada ya kukaa mafichoni kwa muda wa siku sita.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Wiliam Mwampaghale amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema kuwa wanaendelea kumuhoji mtuhumiwa ili jeshi hilo liweze kukamilisha upepelezi kwa ajili ya kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.
“Mtuhumiwa tumemkamata, alienda kujificha katika vichaka kwa muda wote huo na baada ya njaa kali alienda kwa shanghazi yake kuomba chakula na hakumkuta ila aliwakuta watoto waliokuwa wanamfahamu walimuona walipiga kelele na majirani wakafika na kumkamata,” Amesema Mwampaghale.
Kwa mujibu wa taarifa ya familia kijana huyo anayetuhumiwa kwa mauaji alikuwa anaishi na marehemu nyumba moja baada ya mume wa marehemu ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa wa National housing Manispaa ya Bukoba, David Dominick kumchukua na kuishi naye kama mwanafamilia akifanya shughuli za ujenzi akishirikiana na mwenyekiti tangu Novemba,2022.
Tukio la mauji lilitokea Februari 13,2023 majira ya saa 12:00 jioni ambapo mtuhumiwa alimpiga marehemu kwa kutumia silaha butu kichwani upande wa kushoto na kumsababishia jeraha kubwa lililopelekea kuvuja damu iliyomsababisha umauti papo hapo na kisha kumbaka na baada ya kutekeleza tukio hilo aliondoka na kuelekea kusikojulikana hadi alipojitokeza hadharani juzi Jumapili.