Aliyekua Mbunge wa Jimbo La Nchemba (Awali lilifahamika kama Kondoa Kusini) Juma Nkamia ni miongoni mwa wanachama wa klabu ya Simba SC waliojitosa kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa ndani wa klabu hiyo.
Simba SC ipo mbioni kuziba nafasi ya mwenyekiti inayokaimiwa na Mwina Kaduguda ambapo uchaguzi unafatarajiwa kufanyika Februari 07, mwakani (2021).
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Boniface Lihamwike, amesema Nkamia ni sehemu ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo, ili kuziba nafasi ya Swedi Mkwabi aliyejiuzulu mwezi Septemba, mwaka jana.
Lihamwike pia akawataja waliochukua fomu za kuwani nafasi hiyo mpaka sasa ni Hassan Dalali, Ayubu Semvua, Victor Antony, Mohamed Soloka, Kassim Nyangalika, Rashid Shangazi, Piton Mwakisu, Hamisi Omary na Mutaza Mangungu pamoja na mwanahabari mkongwe na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nchemba, Juma Nkamia.
Katika hatau nyingine kiongozi huyo ameongeza kuwa, kamati yake inaendelea na zoezi la utoaji wa fomu za kugombea kwa wanachama ambalo siku hadi siku linaendelea kuchanganya kutoka na wengi wao kupata muitikio wa kutosha kutoa kwenye vyombo vya habari.
“Tunaendelea na zoezi letu la uchukuaji fomu ambalo awali lilianza kwa kulega kutokana na wajumbe kutojitokeza.”
“Tunaamini hadi siku ya mwisho watu wengi zaidi watajitokeza kuchukua fomu ili kutimiza matakwa ya kikatiba ndani ya Simba. Nimekuwa nikipokea simu nyingi sana kutoka kwa wajumbe mbalimbali kuhitaji kuchukua fomu.” Amesema Lihamwike.
Zoezi la uchukuaji fomu linatarajiwa kufungwa Desemba 24, mwaka huu ambapo lilianza Desemba 14.