Mchezaji Mtanzania, Novatus Dismas leo Jumanne (Septemba 19), anaweza kuingia katika rekodi ya kuwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (UCL), wakati timu yake ya Shaktar Donetsk ya Ukraine itakapovaana na FC Porto ya Ureno.
Timu hizo zitakutana katika mechi ya kwanza ya Kundi H itakayochezwa katika Uwanja wa Volksparkstadion, nchini Ujerumani.
Ikiwa Novatus atacheza mechi hiyo, atakuwa Mtanzania wa pili kucheza michuano hiyo baada ya awali, Mbwana Samatta kuweka rekodi hiyo akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji.
Novatus alisajiliwa na Shakhtar msimu huu akitokea Zulte Waregem ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Nyota huyo mwishoni mwa juma lililopita, alikaa benchi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ukraine wakati Shakhtar iliposhinda bao 1-0 dhidi ya FC Obolon Kyiv.
Mechi nyingine ya kundi itakayochezwa leo, itaikutanisha Barcelona ya Hispania dhidi ya Royal Antwerp kutoka Ubelgiji.
AC Milan ya Italia itacheza na Newcastle United ya England katika Kundi F, huku PSG ya Ufaransa iliyopo kundi hilo ikicheza na Borussia Dortmund kutoka nchini Ujerumani.
Katika Kundi E, Feyenoord ya Uholanzi itacheza na Celtic ya Scotland wakati Lazio ya Italia itavaana na Atletico Madrid kutoka nchini Hispania.
Young Boys ya Uswisi itacheza dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani, huku Manchester City ikivaana na FK Crvena Zvezda ya Serbia, zote kutoka Kundi G.