Wananchi na Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wamefurahia elimu na huduma za mfuko huo, zinazotolewa katika maonesho ya tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini kwa mwaka 2022, yaanayoendelea katika viwanja wa uwekezaji (EPZA), Mkoani Geita, kwa kushirikisha Kampuni, Wajasiriamali ,Mashirika na Taasisi mbalimbali za binafsi na Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanachama hao wamesema wamefurahishwa na huduma walizopata katika banda hilo, ikiwemo elimu ya kutumia mifumo mbalimbali ya kidigitali, programu (Applications) za ‘Employer Portal na Member Portal, NSSF Taarifa, NSSF Whatsapp chat bot’ zinazomuwezesha mwanachama na mwajiri kupata huduma popote, jambo ambalo litawapunguzia gharama na usumbufu wa kwenda katika Ofisi za NSSF.
Mmoja wa wananchama hao, Henry Mwinuka amesema, “Nimefurahia Maonesho na pia nimejifunza mambo mengi katika banda la NSSF,nilikuwa sielewi namna ya kuangalia taarifa zangu kwenye simu lakini leo nimepata elimu hiyo na kwamba itapunnguza gharama na usumbufu wa kwenda kwenye ofisini kwao, kwakweli NSSF imejipanga huduma zao ni nzuri hivyo nitoe wito kwa wananchi wanakuja kutembelea maonesho hayo wasisite kuja katika banda la NSSF.”
Naye Mpuzi Masumbuko, mwanachama wa NSSF, amesema, “Nimekuja hapa kuangalia taarifa zangu za michango kama mwajiri wangu ananiwekea katika Mfuko,sasa nimekuja hapa katika Maonesho nikadhani ni bora nije kuangalia taarifa za michango yangu nimekuta ziko vizuri mwajiri wangu anaweka michango yangu kwakweli nimefurahi na nimeridhika na huduma nilizopata hapa.“
Licha ya Mfuko huo, kutoa huduma mbalimbali za Hifadhi ya Jamii, pia unasajili wanachama wapya baada ya kuwapatia elimu kupitia mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa sekta isiyo rasmi, ambapo wananchi waliojiajiri wenyewe wakiwemo wachimbaji wadogo wadogo wa madini wanapata fursa ya kujiwekea akiba ya baadaye.
“Maonesho haya ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini hapa Mkoani Geita yamenipa fursa kuja katika banda la NSSF kujiunga na hivyo nashukuru nimefanikisha kuwa mwanachama wa NSSF, sasa nitaanza kujichangia kwa hiari nijiwekee akiba, hii ni kama kibubu cha kisasa si kama kile kilichokuwa nyumbani mwisho wa siku kinabomolewa,” amesema mwanachama mpya wa NSSF, Festus Mluli.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu, ‘Madini na fursa za kiuchumi: Ajira kwa Maendeleo Endelevu’, yalianza tarehe 27 Septemba 2022 ambayo yanafanyika Mkoani Geita, yanatarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 8, 2022.