Uongozi wa klabu ya Young Africans umesema kuwa licha ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Azam FC uliochezwa Jumapili (April 25) Uwanja wa Benjamin Mkapa, bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika michezo ijayo na hawajakata tamaa.
Katika mchezo huo Young Africans walikubali kuchapwa bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Mpumelelo Dube dakka 85, na kuifanya klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kusalia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, wakitanguliwa na Simba SC.
Afisa Uhamasishaji wa Young Africans Antonio Nugaz, amesema kuwa ni matokeo mabaya ambayo wameyapata, na tayari benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Nasrideen Al Nabi, limeanza kuyafanyia kazi makosa yaliyopelekea kichapo hicho.
Amesema kupoteza mchezo dhidi ya Azam FC hakujawakatisha tamaa wao kama viongozi, hivyo anaamini hali hiyo ipo kwa wanachama na mashabiki ambao wamekua bega kwa bega na kikosi chao, tangu mwanzoni mwa msimu huu, ambapo kilikua kiifanya vyema kwenye michezo ya Ligi Kuu.
“Hakuna kukata tamaa. Tuendelee kupambana kwenye kila mchezo kwa kila namna ibakie matokeo ya mpira na bahati ya siku yenyewe.”
“Hapa lengo letu ni moja tu! kuendelea kupambana hadi pumzi yetu ya mwisho, na IN SHAA ALLAH tunaamini tutapata tunachokikusudia, na hicho sio kingine zaidi ya ubingwa wa Tanzania Bara ambao tumeumiss kwa misimu mitatu mfululizo.” Amesema Nugaz
Ushindi wa bao moja kwa sifuri, umeiwezesha Azam FC kufikisha alama 54 ikiwa nafasi ya tatu huku Young Africans ikibaki na alama 57 zinazowaweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo na Simba SC mwenye alama 58 wanaongoza msimamo huo kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu 2020/21.