Wakati zaidi ya robo tatu ya watu wazima wote wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), wanapata aina tofauti za matibabu, idadi ya watoto wanaopatiwa huduma hiyo inafikia asilimia 52 pekee na kufanya watoto wengi kuwa nje ya matibabu ya ugonjwa huo.
Katika kukabiliana na tofauti hiyo, mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa kwakushirikiana na wadau wengine wameunda ubia wa kimataifa ili kuzuia maambukizi mapya ya VVU, na kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 watoto wote walio na VVU wanaweza kupata matibabu ya kuokoa maisha.
Taarifa iliyotolewa leo katika miji ya Montreal – Canada, Geneva – Uswisi na New York – Marekani, imeyataja mashirika hayo kuwa ni lile linashughulika na masuala ya UKIWMI UNAIDS, la watoto UNICEF na la afya ulimwenguni WHO, ambayo kwa pamoja yanashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa, asasi za kiraia na serikali kufanikisha mpango huo.
Muunganiko huo, umetangazwa katika Mkutano wa kihistoria wa Kimataifa wa UKIMWI, ambao unafikia tamati mjini Montréal, Canada, hii leo Agosti 3, 2022 na kutaja nchi 12 zilizojiunga na ubia katika awamu ya kwanza kuwa ni Angola, Cameroon, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Msumbiji, Nigeria, Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda, Zambia na nyumbani Tanzania.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, DkT. Tedros Adhanom Gheberyesus amesema hakuna mtoto anayepaswa kuzaliwa na VVU au kukua na VVU, na hakuna mtoto aliye na VVU anayepaswa kutopata matibabu.
Amesema, “Ni ukweli kwamba nusu tu ya watoto wenye VVU wanapokea dawa za kurefusha maisha, hii ni kashfa na doa katika dhamiri zetu za pamoja. Ubia wa Kimataifa wa Kutokomeza UKIMWI kwa Watoto ni fursa ya kufanya upya ahadi yetu kwa watoto na familia zao kuungana, kuzungumza na kutenda kwa nia na mshikamano na akina mama wote, watoto na vijana.”
Katika mkutano huo, Waziri wa Afya wa Nigeria Dkt. Osagie Ehanire, aliahidi kubadilisha maisha ya watoto walioachwa bila huduma hiyo, kwa kuweka mifumo inayohitajika ili kuhakikisha kuwa huduma za afya zinakidhi mahitaji ya watoto wanaoishi na VVU.
Nchi ya Nigeria, itakuwa mwenyeji wa uzinduzi wa kisiasa wa muungano huo barani Afrika katika mkutano wa Mawaziri utakaofanyika jijini Abuja Oktoba 2022.