Kamanda wa polisi Mkoa walindi ACP John Makuri amesema sababu mojawapo iliyochangia ongezeko la vifo baada ya kutokea ajali ya Basi la Baraka Classic lililokuwa linatokea Wilayani Newala Mkoani Mtwara kuelekea jijini Dar es salaam ni Nyuki walioanza kung’ata watu hivyo kushindwa kutoa msaada kwa haraka.

Kamanda Makuri ameyasema hayo wakati akizungumzia tukio la ajali hiyo iliyotokea eneo la Mputa maarufu kama kona ya Nyale lililopo Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi ambapo watu 14 walipoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa baada ya Basi hilo lenye namba ya usajili T336 DPW, kufeli breki na kuanguka.

Amesema, “vifo 12 vilikuwa ni vya abiria waliokuwa ndani ya basi hilo na vifo vya watu wawili ni wale waliokuwa wakitembea kwa miguu na majeruhi wapo 26 wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Nyangao na Dereva wa Basi la Baraka naye anapatiwa matibabu katika Hosptali hiyo ya Nyangao akiwa chini ya ulinzi.”

Akizungumzia ajali hiyo na suala la Nyuki kung’ata watu, Diwani wa kata na Halmashauri ya Mtama, Maria Nyale amesema,
“baada ya ajali Nyuki walitimka sana ikasababisha kushindwa kuwaokoa watu lakini Polisi walifika mapema wakashirikiana na wananchi kuchoma mipira nyuki wakatoka na zoezi la uokoaji likaendelea.”

Benchikha awachimba mkwara wachezaji Simba SC
FC Barcelona yakanusha mpango wa Gundogan