Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo amesema kuwa Wananchi wa vijijini wasiwe na taharuki nyumba zilizojengwa kwa vifaa ambavyo sio vya kudumu hazitahusika na kodi za majengo.
Amesema hayo leo Agosti 23 kupitia kipindi cha Clouds360 kinachorushwa Clouds Tv kuhusu mfumo mpya wa ulipaji wa kodi ya majengo.
“Naomba niweke wazi Wananchi wasiwe na taharuki nyumba za Vijijini haziko katika mpango wa kutozwa kodi ya majengo vilevile nyumba zilizojengwa kwa vifaa ambavyo sio vya kudumu kama zile udongo zilizoezekwa kwa nyasi hazihusiki na kodi ya majengo.” Amesema Kayombo.
Kayombo ameeleza kuwa kodi ya majengo ni kodi ambayo inatozwa kutokana na maendeleo ya juu ya ardhi, mara nyingi watu wanaichanganya na kodi ya ardhi, kodi ya ardhi inalipwa Wizara ya ardhi.
Aidha amesema kuwa kodi ya pango la ardhi ni ardhi ambayo haina chochote au ina chochote, kodi ya jengo ni yale maendelezo juu ya hiyo ardhi inaweza ikawa jengo au muundo wowote wa ujenzi.
Kayombo amesema kodi ya majengo awali ilikuwa ikikusanywa na Serikali za mtaa, baadaye ikahamishiwa TRA, sasa inakusanywa kupitia manunuzi ya luku mfumo ambao unarahisisha ufanisi na ukusanyaji wa kodi kwa gharama nafuu.