Wakati serikali ikiendelea kupambana na nzige wavamizi katika Wilaya ya Longido, kundi jingine la nzige hao limevamia katika wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wilayani Siha wakati alipotembelea kujionea kundi hilo, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda amesema licha ya kundi hilo kuwa dogo, Wizara itahakikisha inaangamiza makundi yote ya nzige kwa kuua mazalia yake ili wasiweze kuzaliana.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelo amesema nzige hao kwa sasa wako katika mashamba ya Namwai, Felician, Kanamodo na Kafoi katika kata ya Ngarenairobi ambapo hakuna madhara katika mashamba ya wananchi licha ya kuwa kwa sasa mazao yameanza kuoteshwa.
Baadhi ya wakulima wamesema wakati nzige hao wanaingia waliingiwa na hofu lakini wanaishukuru serikali kwa jitihada wanazozichukua katika kupambana na wadudu hao.