Kiasi cha Euro milioni 157, zimetengwa kwa ajili ya kuwakopesha wadau wa kilimo ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibeani na Pasifiki (OACPS), kama njia mojawapo ya kuwekeza kwenye sekta hiyo na kuongeza thamani ya mazao.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amesema hayo ni moja kati ya mazimio yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS, uliofanyika Juni 8 – 9, 2022 jijini Brussels nchini Ubelgiji.
Amesema, wadau wa kilimo nchini wanaotaka mikopo hiyo nafuu watatakiwa kutuma maombi kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, na kuweza kushiriki kikamilifu katika mkakati huo wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo.
“Tumeanzisha mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo, na ili kufanikisha azimio hilo Jumuiya imetenga Euro milioni 157 ambazo zitatoka kama mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima ndani ya jumuiya yetu ya OACPS” alisema Balozi Sokoine.
Balozi Sokoine, ambaye alimuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika mkutano huo, ameyataja maazimio mengine kuwa ni Tanzania kupewa nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya masuala ya Uvuvi kwa miaka miwili, kuanzia 2022 hadi 2024.
“Hatua hii ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kusimamia utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa buluu na kukuza ushirikiano baina ya nchi za OACPS katika sekta ya uvuvi uenyekiti huu umetufanya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa masuala Uvuvi unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.” alisema.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa OACPS, ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya kinachohusika na utekelezaji wa maazimio, yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.