Mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio Raila Odinga hatimaye amewasilisha rasmi ombi la kupinga Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Urais ambapo William Ruto aliibuka na kuwa mteule.
Mawakili wawili wa Raila Odinga walioongozwa na wakili James Orengo waliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya upeo ya Milimani na tayari kimewasilisha kesi hiyo mtandaoni na kwamba watawasilisha stakhabadhi zinazohitajika mahakamani wakati wowote.
“Tumewasilisha kesi hiyo kupitia mtandao huku tukisubiri kuleta stakhabadhi ili mahakama hiyo iweze kuthibitisha ombi hilo, Tuna hadi saa nane lakini naweza kuwahakikishia kwamba kila mtu yuko tayari. Kundi la mawakili linaendelea kukusanya nakala za kesi hiyo na zinatarajiwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa”, alisema wakili wa Muungano wa Azimio Daniel Maanzo.
Sheria kuhusu kesi ya kupinga uchaguzi wa Urais 2017 inasema iwapo kesi itawasilishwa katika siku ya mwisho ya muda uliowekwa wa kuwasilisha kesi, basi lazima ifanyike kabla ya saa nane mchana katika siku hiyo.
Kufuatia hatua ya kuwasilisha kesi hiyo mahakamani, Muungano wa Azimio una hadi tarehe 23 Agosti, kukikabidhi chama cha UDA, rais Mteule na tume ya uchaguzi IEBC malalamishi hayo.
Matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi IEBC yalisema kwamba Mgombea wa chama cha UDA ndiye aliyeshinda uchaguzi kwa asilimia 50.49 huku mpinzani wake wa karibu Raila Odinga akipata asilimia 48.85.
Hii ni mara ya tano kwa Raila Odinga kuwania wadhifa huo ikiwa Mwaka 2017, mahakama ya upeo iliagiza marudio ya uchaguzi , uchaguzi ambao ulisusiwa na Odinga ambaye alipoteza tena kwa rais aliyepo madarakani Uhuru kenyatta.
Hata hivyo wafuasi wa Muungano wa Azimio wamekongamana nje ya mahakama hiyo ya milimani na usalama umeimarishwa nje ya mahakama hiyo.