Beki wa Azam FC Nathaniel Chilambo amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kutajwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kilichoingia kambini leo Jumatatu (Agosti 22).

Taifa Stars imeanza kambi jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.

Chilambo aliyesajiliwa Azam FC miezi miwili iliyopita akitokea Ruvu Shooting, amesema amefarijika kuwa sehemu ya kikosi kilichoitwa na Kocha Kim Poulsen mwishoni mwa juma lililopita, kwani ilikua ni sehemu ya ndoto zake kuitumikia ‘Taifa Stars’.

Amesema dhamira yake kubwa baada ya kuitwa kwenye kikosi hicho ni kupambana ili aingie kwenye kikosi cha kwanza kitakachokuwa na kazi kubwa ya kuitetea nchi kwenye harakati za kufuzu Fainali za CHAN.

“Ni ndoto iliyotimia, tangu nikiwa mdogo nilikua na shauku ya kutaka kuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars, leo ninahisi furaha kuwa sehemu ya wachezaji walioripoti kambini na kuanza mazoezi kwa ajili ya mchezo wa Kimataifa dhidi ya Uganda.”

“Naamini kila mchezaji wa Tanzania anatamani nafasi hii ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, kazi kubwa niliyonayo sasa ni kupambana ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza, ili kuweza kuwa sehemu ya watu watakaoandika historia ya kuivusha nchi na kutinga kwenye Fainali za CHAN.”

“Binafsi nipo tayari kulipambania taifa langu, ninaamini kwa kushirikiana na wenzangu, tutafanikiwa kufikia lengo la kushinda dhidi ya Uganda.” amesema Chilambo

Stars iliitoa Somalia katika mchujo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1, ilishinda 1-0 kisha ikaibutia 2-1.

Kenya: Odinga atinga Mahakamani 'kibabe' na Lori la ushahidi
Kim Poulsen: Nitatuzitumia siku sita kikamilifu