Baada ya mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’ kushinda zabuni ya uwekezaji ndani ya Klabu ya Simba ambapo kutakuwa na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kutoka uanachama hadi hisa, kuna ufafanuzi ambao umekuwa ukiwachanganya wengi.
Msajili wa vyama vya michezo nchini Tanzania, Ibrahim Mkwawa ametoa ufafanuzi juu ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kwa klabu zilizoanzishwa na wanachama kwenda kwenye mfumo wa hisa kama ilivyofanya Klabu ya Simba.
Msajili huyo ameeleza kwamba, kanuni mpya za serikali zilizotoka Oktoba 2017 zinaeleza kwamba mfumo wa hisa ni asilimia 51 kwa 49.
Amesema kanuni hizo zimeshakuwa sheria ambapo zinaeleza kuwa kila klabu iliyoanzishwa na wanachama inapaswa kutenga asilimia 51 kwa ajili ya wanachama wake na asilimia 49 kwa ajili ya mwekezaji.
Amedai kuwa kama Simba hawakuliweka wazi suala hilo siku ya mkutano ni juu yao lakini huo ndiyo uhalisia wa kanuni.
Amesisitiza kuwa wanachama na mashabiki wa mpira waelewe kwamba, serikali sasa imeshatunga kanuni ambazo itaziongoza klabu zote na siyo Simba pekee.
Ufafanuzi huo umekuja baada ya kuwepo madai kuwa Mo Dewji atamiliki hisa kwa asilimia 50 au zaidi baada ya mabadiliko hayo kupitishwa.
Mwekezaji anapokuwa na hisa zaidi ya 50 inamaanisha ndiye anayekuwa mmiliki mwenye nguvu kuliko wengine wote katika klabu, lakini kwa mfumo huo wa Serikali inamaanisha bado wanachama watakuwa na nguvu ya umiliki wa klabu yao.