Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na Klabu ya Simba SC ya Tanzania Augustine Okrah, amesema yupo tayari kwa mapambano ya kuisadili klabu hiyo kurejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania Bara na kufika mbali katika michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Okrah alitambulishwa jana Jumatano (Julai 13) kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kupitia Simba APP na Kusaraza za Mitandao ya Kijamii za klabu hiyo ya Msimbazi, baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili wake.
Kiungo huyo mwenye sifa ya kukimbia na chenga za maudhi, amesema amekuja Tanzania kufanya kazi na hana budi kujifananisha na Mwanajeshi aliye vitani, ambapo muda wote anapaswa kuwa tayari kwa mapambano.
Amesema hajali Miundombinu, Lugha ama Mazingira mengine ambayo huenda yakawa changamoto kwake, kikubwa anajua amekuja Tanzania Kufanya kazi na Simba SC inayohitaji kurejesha Ubingwa wake na kufika mbali kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao.
“Ukiwa askari ni lazima uwe tayari kila wakati, hivyo kila ninapoenda uwanjani najituma kwa kadri ya uwezo wangu. Sitaangalia miundombinu ikoje, lugha… nipo hapa kufanya kazi kwa bidii na kujitolea kwa kadri niwezavyo kwa ajili ya klabu.” amesema Okrah
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, anatarajiwa kuwa sehemu ya Kikosi cha Simba SC kitakachoondoka jijini Dar es salaam leo Alhamis (Julai 14), kuelekea Ismailia-Misri kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya Msimu Mpya.