Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Nigeria Nelson Okwa anaamini mabadiliko ya Benchi la Ufundi Simba SC, ndio sababu kubwa inayomfanya kushindwa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.
Simba SC ilifanya mabadiliko ya Benchi la Ufundi, baada ya kuachana na Kocha Zoran Maki kutoka Serbia na nafasi yake kuchukuliwa na Kocha mzawa Juma Ramadhan Mgunda mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Okwa aliyesajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United, amesema anaamini mfumo wa Kocha Zoran Maki ulimpa nafasi ya kuwa sehemu ya wachezaji waliotumika kwa wakati huo, lakini uwepo wa Kocha Mgunda kwa sasa umekua kikwazo, lakini hajakata tamaa.
“Nilipata nafasi chini ya Kocha Zoran Maki, wakati huo pia kuna baadhi ya wachezaji walikua hawapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi, mfano mzuri ni kama Mzamiru Yassin, Joash Onyango na wengine,”
“Ninaamini utafika muda nitacheza na nitaonyesha uwezo mkubwa na kutoa mchango wa kuisaidia timu yangu kupata matokeo mazuri uwanjani,”
“Unajua kila kocha ana aina ya wachezaji anaowahitaji kutokana na mfumo wake, anaweza kuhitaji mchezaji anayekimbia sana, anayejua kukokote mpira na kutoa pasi, anayejua zaidi kufunga, naamini wanaopata nafasi kwa sasa wanafit kwenye mfumo ambao Kocha Mgunbda anautumia kwa sasa,”
“Naamini utafika wakati hata mimi nitaingia katika mfumoa mbao atautumia mbele ya safari kwa sababu msimu ni mrefu na tutacheza michezo mingi itakayokua na changamoto tofauti.” amesema Okwa