Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha leo Juni 2, 2021 itasikilizwa kesi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na walinzi wake watano, ambao wanakabiliwa na mashtaka sita na mawili ya ujambazi wa kutumia silaha.
Mashitaka mawili ambayo leo yanatarajiwa kuanza kusikilizwa ni ya ujambazi wa kutumia silaha ambayo mawakili wa Serikali, Tumaini Kwema, Abdallah Chagula na Tarsila Garvas wameeleza kuwa upelelezi wake umekamilika.
Mashitaka hayo yatafikishwa leo mbele ya mahakimu wawili tofauti ambao ni Hakimu Mfawidhi, Martha Mahumbuga na Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha.
Wakisomewa maelezo ya makosa hayo Juni 18, Wakili Gervas alidai Februari 9, mwaka huu, Sabaya na watuhumiwa wawili, Silivester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38) walivamia duka la Mohamed Saad, lililopo mtaa wa Bondeni.
Hatahivyo Gervas alidai kuwa watuhumiwa hao walitumia silaha, ambayo ni kinyume cha kifungu cha 287(a) cha mwenendo wa makosa ya jinai, kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Hata hivyo, watuhumiwa hao baada ya kusomewa mashitaka hayo, walikana na Hakimu Mfawidhi, Salome Mshasha aliahirisha kesi hiyo hadi leo, Julai 2.
Katika makosa mengine manne, Sabaya na walinzi wake wanne, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38), Enock Mnkeni (41), Watson Stanley (27) na John Odemba Aweyo maarufu kwa jina la Mike One, walisomewa mashtaka manne ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, kuunda genge la uhalifu na kuomba rushwa.