Kikosi cha KMC FC kimeendelea kujiweka vizuri kuelekea katika mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara dhidi ya Simba kwa kucheza mechi nyingine leo ya kirafiki dhidi ya Timu ya Transit Camp ya Jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa magoli matatu kwa sifuri.

Kupitia mchezo huo wa kirafiki , KMC FC iliyopo chini ya Makocha, Kocha Mkuu John Simkoko pamoja na Habibu Kondo inajiandaa vikali kwa mchezo ambao utapigwa Julai 7 mwaka huu katika Uwanja wa Benjamini Mkapa saa 19:00 usiku.

Mchezo huo ambao KMC FC wamecheza saa mbili kamili asubuhi katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, magoli yamefungwa na wachezaji Matheo Antony ambaye amefunga magoli mawili huku goli la tatu likifungwa na Hassan Kapalata.

Michezo hiyo ni mahususi kwa ajili ya kuiandaa Timu katika michezo mitatu iliyosalia ikiwemo ya Simba ambapo Makocha wanaendelea kutumia michezo hiyo kwa lengo la kukiweka kikosi vizuri sambamba na kusawazisha makosa mbalimbali na hivyo kupata matokeo mazuri ikiwemo kuondoka na alama tatu kwenye mchezo muhimu dhidi ya wakundu hao wa msimbazi.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, imejipanga kuhakikisha kwamba licha ya ushindani uliopo kwa Timu ya Simba lakini bado kikosi hicho cha wana Kino Boys kinajipanga kupambana ili kuibuka na ushindi na hivyo kuchukua alama tatu dhidi ya Simba.

Jana KMC FC ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba ya Mkoani Mwanza ambao ulipigwa saa mbili kamili asubuhi katika Uwanja wa Uhuru Jijini hapa na kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sifuri ambayo yalifungwa na wachezaji, Crif Buyoya pamoja na Kevin Kijili.

Imetolewa leo Julai 2

Na Christina Mwagala

Afisa habari na Mahusiano wa KMC FC

Kesi ya sabaya yafika hapa leo
Ole Sabaya Mahakamani tena