Mkuu wa TPF NET Mkoa wa Kusini Pemba, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Habiba Ali Said amewataka wanafunzi kujiepusha na vitendo vitakavyowapelekea kufanyiwa udhalilishaji, hali ambayo itawasababishia kufa kwa ndoto zao kimaisha.
Akizungumza na wanafunzi wa Skuli za Michaini A na B, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, Inspekta Habiba amewataka Wanafunzi hao kuacha tabia za kuomba lifti, kuomba pesa za matumizi, kupokeza zawadi kwa watu wasiowafahamu.
Amesema, “Lakini pia mjiepushe na watu wasio na tabia njema msikubali kuitwa wachumba au mpenzi na mkiona viashiria au hali kama hiyo toeni taarifa mapema, mtakapoona mtu anayetaka kuwafanyia kitendo viovu fanyeni haraka ili kupata msaada na hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Aidha, amewataka Wanafunzi hao pia wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika masomo yao, ili waweze kuzifikia ndoto na malengo yao kwani kukubali, kupuuzia au kuendekeza vitendo hivyo ni kujiharibia mfumo wa masomo na maisha.