Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Wekundu wa Msimbazi Simba Joash Onyango Achieng, amewapongeza Young Africans kwa kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi 2021.
Onyango ambaye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao uliunguruma Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja-Zanzibar jana Jumatano (Januari 13), amesema hana budi kutuma salamu za ubingwa, kutokana na kitendo hicho kubeba dhana ya uungwana katika michezo.
Beki huyo kutoka Kenya amesema dhamira ya kikosi cha Simba ilikua ni kutwaa taji la Mapinduzi 2021, lakini haikua bahati yao licha ya kupambana ndani ya dakika 90, na hatimae kuangushwa kwenye changamoto ya mikwaju ya penati.
“Mchezo ulikua mzuri, pande zote mbili zilikua zimejipanga na ndio maana tulicheza ndani ya dakika 90 na mshindi hakupatikana, lakini kwenye penati wenzetu wametushinda,”
“Kama ilivyo kawaida katika penati huwa hakuna mwenyewe, na ndivyo ilivyokua kwetu, tumeshindwa na hatuna budi kujipanga kwa michezo mingine inayofuata kwa msimu huu.”
“Tutakwenda kurekebisha makosa yetu, natumai katika michezo mingine tukikutana na mpinzani kama Young Africans tutaweza kufanya vizuri.” Amesema Onyango ambaye alikosa mkwaju wa penati, akitanguliwa na Meddie Kagere.
Young Africans inayonolewa na kocha kutoka nchini Burundi Cedric Kaze imetwaa taji la pili la kombe la Mapinduzi katika historia ya michuano hiyo, baada ya kufanya hivyo mwaka 2007.