Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameitangaza leo, Februari 23 kuwa siku maalum ya kufunga na kuziombea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini.
Nchi hizi zimekuwa katika hali mbaya ya kisiasa na vita zinapelekea uvunjifu wa haki za binadamu, mauaji ya watu wasio na ongezeko la wakimbizi hali iliyosababisha kiongozi huyo kuomba Roho Mtakatifu aingilie kati.
Aidha, Papa amewataka waumini wa dini nyingine pia kuungana katika maombi hayo, wito ambao umeitikiwa kwa mikono miwili na kiongozi wa kanisa la Anglican, Justin Welby ambaye ameeleza kile alichokishuhudia alipotembea nchi hizo.
“Katika ziara yangu ya hivi karibuni kwa nchi hizo mbili, nilishuhudia uharibifu mkubwa uliofanyika ambao hauwezi kuelezeka. Migogoro hii inasababisha maisha ya watu kupotea. Idadi kubwa ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao hali inayovunja familia na jamii,” alisema Welby.
Welby alieleza kuwa katika maombi ya leo, watu wanapaswa kuwaombea viongozi wa Sudan Kusini na Kongo kubadili mioyo yao kutoka kwenye vita kuwa katika amani.