Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa msaada wa kiasi cha Dola 121,000 sawa na Pauni 90,000 kwa ajili ya kusaidia wahanga wa mashambulio ya kigaidi yaliyotokea kaskazini mwa Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado.
Msaada huo umetolewa baada ya Askofu wa Pemba, Luis Fernando Lisboa, kuomba msaada kwa ajili ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia za wanamgambo wa Kiislamu.
Maombi hayo ya askofu yalitaka suluhisho la kiusalama na msaada kwa watu waliopoteza makazi yao.
Akiongoza kampeni inayofahamika kama “Together for Cabo Delgado” yaani Pamoja kwa ajili ya Cabo Delgado, Askofu Lisboa amewaambia waandishi wa habari kuwa Papa ametuma mchango wake ambao utatumika kujenga hospitali na makazi ya watu ambao wanaishi katika kambi haswa katika eneo la Montepuez na Chiure.
Takriban watu 430,000 wameachwa bila makazi kutokana na vurugu hizo ambazo zimekuwapo katika maeneo yenye utajiri wa gesi tangu mwaka 2017.