Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis anatazamiwa kukutana na viongozi wakuu wa dini ya Kiislamu, akiwa katika ziara nchini Bahrain inayoazimia kuboresha mjadala baina ya imani tafauti.
Papa Francis aliwasili jana (Novemba 3, 2022) katika taifa hilo la Ghuba ya Arabuni na kutoa hotuba iliyokosoa adhabu ya kifo na kuhimiza mataifa kuheshimu haki za binaadamu na kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi.
Makundi ya kutetea haki za binaadamu, yamemtaka Papa kuangazia madai ya unyanyasaji unaofanywa na ufalme wa Bahrain, unaoongozwa na wafuasi wa madhehebu ya Sunni katika taifa hilo ambalo raia wengi ni wa madhehebu ya Shia.
Leo Ijumaa (Novemba 4, 2022) Papa Francis anakutana na Imam mkuu wa msikiti wa Al-Azhar wa mjini Cairo Misri, Sheikh Ahmed al-Tayeb, ambacho ni kituo kikuu cha mafunzo ya madhehebu ya Sunni.
Papa Francis ameufanya mjadala baina ya dini tofauti kuwa kiini cha uongozi wake, na amezizuru nchi kadhaa za Kiislamu zikiwemo Uturuki, Misri na Irak.