Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameomba radhi kwa kitendo cha kumpiga kofi mwanamke mmoja aliyekuwa ameung’ang’ania mkono wake nje ya eneo la Kanisa la St. Peter’s Square, Jumanne, Desemba 31, 2019 jijini Vatican.
Papa Francis alikuwa anatembea mbele ya waumini waliokuwa wamefurika, ambao mwanamke huyo alimshika mkono na kumng’ang’ania kitendo kilichomkasirisha kiongozi huyo wa kanisa Katoliki na akampiga kofi juu ya mkono wake.
Akizunguma Januari Mosi, kwenye ibada ya kufungua mwaka, Papa Francis amehubiri kuhusu kukomesha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na akaomba radhi kwa mfano mbaya aliouonesha jana.
“Upendo huleta uvumilivu. Kwahiyo, mara nyingi tunakosa uvumilivu, hata mimi, na ninaomba radhi kwa kuwa mfano mbaya jana,” alisema Papa Francis mwenye umri wa miaka 83.
“Wanawake ni chanzo cha maisha. Lakini wameendelea kuonewa, kupigwa, kubakwa na kulazimishwa kuwa makahaba na kuyatoa maisha yao… haya matendo ya unyanyasaji ni kinyume na matakwa ya Mungu,” aliongeza.
Mwanamke huyo aliyemng’ang’ania mkono ambaye kabla alikuwa akionesha ishara ya msalaba alikuwa anazungumza mambo ambayo hayakusikika kwenye vipande vya video vilivyochukuliwa kutokana na kelele za umati.