Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Young Africans Mwinyi Zahera, amerejea Ligi kuu Tanzania Bara, baada ya kutangazwa kuwa kocha mkuu wa Gwambina FC usiku wa kuamkia leo.
Gwambia FC ambao watashiriki Ligi Kuu msimu ujao 2020/21, wamemtangaza kocha huyo wakiamini atawezesha safari ya mafanikio ya kufanya vyema kwenye Mshike Mshike wa soka la Bongo. Gwambina FC imepanda daraja msimu huu wa 2019/20, ikitokea ligi daraja la kwanza.
Zahera amesaini dili la awali kabla ya kutimiza vigezo alivyopewa, huku akitajwa kuanza na ishu ya usajili wa wachezaji katika kipindi hiki cha Dirisha kubwa ambalo litafungwa rasmi mwishoni mwa Mwezi Agosti.
Kuajiriwa kwa kocha huyo kutoka DR Congo, kunatajwa kama kichocheo cha kusajiliwa kwa wachezaji waliowahi kucheza Young Africans Mrisho Ngasa, Juma Abdul na Kelvin Yondani ambao kwa sasa ni wachezaji huru.
Zahera aliwahi kuifundisha Young Africans msimu wa 2018/19 na alianza nayo msimu wa 2019/20 kabla ya kufungashiwa virago kwa kile kilichoelezwa kuwa aliboronga kwenye michuano ya kimataifa.