ocha Mkuu wa Tanzania Prisons Patrick Odhiambo amesema ana kazi kubwa ya kufanya dhidi ya JKT Tanzania, baada ya kikosi chake kushindwa kupata nafasi ya kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao (2022/23).
Tanzania Prisons itacheza mchezo wa ‘Play Off’ dhidi ya JKT Tanzania Jumamosi (Julai 09) jijini Dar es salaam, baada ya kupoteza dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo kama huo wa Ligi Kuu kwa kukubali kichapo cha jumla cha 3-2.
Odhiambo amesema kikosi chake kitalazimika kupambana kwa nguvu na akili dhidi ya JKT Tanzania, kufuatia wapinzani wao kuwa na uezofu wa kutosha katika michezo inayohitaji matokeo ya kusonga mbele.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya, JKT Tanzania wana uzoefu mkubwa sana katika michezo kama hii, nina uhakika mchezo utakua mgumu sana, hivyo sina budi kujiandaa na kukiandaa kikosi changu ili kwenda kupambana ugenini kabla ya kumalizia nyumbani.”
“Ninafahamu umuhimu wa kushinda mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania, ninaamini hata wao wanajua umuhimu huo, hapo ndipo kutakapoleta ushindani na ugumu wa mchezo tutakaocheza kwa pamoja, lakini nitajiandaa kwa kusaka ushindi.” Amesema Odhiambo
Kanuni zimeishuka timu hiyo ya Maafande wa Jeshi la Magereza kucheza na JKT Tanzania inayotoka Ligi Daraja la Kwanza, baada ya kushindwa mchezo wake wa kujitetea kubaki Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Tanzania Prisons ilipoteza dhidi ya Mtibwa Sugar nyumbani Sokoine jijini Mbeya kwa 3-1 na jana Jumatano (Julai 06) ilipata ushindi wa 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
JKT Tanzania ilicheza mchezo wa ‘Play Off’ wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Kitayose FC ya Tabora. Katika mchezo wa Mkondo wa kwanza uliopigwa Dar es salaam JKT Tanzania ilichomoza na ushindi wa 2-0, kabla ya kulazimisha sare Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi Tabora ya 1-1.