Kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba huenda akawa nje ya uwanja kwa majuma kadhaa, kufuatia majeraha aliyoyapata usiku wa kuamkia leo, wakati wa mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi dhidi ya FC Basel.
Jose Mourinho aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kuwa, Pogba anahofiwa kuwa na majeraha katika sehemu za paja lake, ambayo yalimzuia kuendelea na mchezo huo, uliomalizika kwa Man Utd kupata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
Pogba alilazimika kutoka nje ya uwanja dakika ya 18 na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo kutoka nchini Ubelgiji Marouane Fellaini aliefunga bao la kwanza.
“Sifahamu lolote kuhusu ukubwa wa jeraha lake. Lakini kwa uzoefu wangu huenda akawa amepata maumivu wa misuli ya paja, na kwa kawaida matatizo hayo humuweka mchezaji nje ya uwanja kwa majuma kadhaa,” Mourinho aliwaambia waandishi wa habari.
“Lakini inatubidi kusubiri majibu ya vipimo atakavyofanyiwa kesho (leo) ili kufahamu zaidi ukubwa wa tatizo la Pogba.”
Kufuatia hali hiyo, Pogba ana asilimia kubwa ya kuukosa mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya Everton utakaochezwa mwishoni mwa juma hili, katika uwanja wa Old Trafford.
“Hatuwezi kuanza kulia kwa sababu ya majeraja yanayomkabili Pogba. Kwa sababu ni jambo la kawaida kutokea katika michezo, kuhusu jumapili kama atashindwa kucheza, nina wachezaji wengine wenye uwezo wa kuziba nafasi yake kama Herrera, Carrick, Fellaini na Matic.”.
Mwishoni mwa juma lililopita Man Utd walipunguzwa kasi ya kushinda michezo michezo yao ya awali, baada ya kulazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili na Stoke City, huku wapinzani wao wa jumapili Everton wakiwa wameshinda mchezo mmoja kati ya michezo minne waliyocheza tangu mwanzo wa msimu huu.