Aliyewahi kuwa Nahodha na Beki wa Simba SC Boniface Pawasa ametoa ushauri kwa uongozi wa timu hiyo kuhakikisha wanalitumia vizuri dirisha kubwa la usajili kusajili wachezaji wenye viwango bora watakaoweza kukidhi mahitaji ya timu.
Uongozi wa Simba SC umedhamiria kufanya usajili mkubwa na mzuri ili kufanikisha lengo la kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika Nusu Fainali ama Fainali katika Michuano ya Kimataifa msimu ujao 2023/24.
Pawasa ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya ufukweni ameeleza kuwa uongozi na benchi la ufundi wa timu hiyo wanapaswa kufanya tathmini baada ya msimu kumalizika, kuangalia aina ya wachezaji wanaostahili kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.
“Bidhaa ya Simba SC ni ubora wa kikosi chao na siyo majengo, jezi nzuri au uwanja.
“Mafanikio ya timu ni matokeo ya uwanjani hapo utaona mashabiki wanajaa uwanjani na makombe yanatua kila msimu,” amesema Pawasa
Kocha huyo amesema kama mchezaji wa zamani wa Simba SC, anauheshimu uongozi wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi lililopo chini ya Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’, angeshauri kuangalia sehemu muhimu kwenye usajili kama beki wa kati na eneo la ushambuliaji kwa kupata mtu sahihi.