Mshambuliaji kutoka nchini Norway na Klabu ya Manchester City Erling Haaland anaongoza katika orodha ya wachezaji wenye thamani kubwa duniani wakati wachezaji wawili wa England pekee wakiwamo kwenye 10 bora.

Nyota huyo mwenye miaka 22 amekuwa na rekodi bora katika msimu wake wa kwanza akiwa na Manchester City akifunga mabao 52.

Mchezaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ameshatwaa taji la Ligi Kuu England, kabla ya kuisaidia timu yake kuifumua Manchester United mabao 2-1 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA, kwenye Uwanja wa Wembley, wiki iliyopita.

Ni Inter Milan pekee iliyobaki katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumamosi, ambayo Cityzens inaweza kuibuka na mataji matatu ya msimu mmoja (Treble).

Na katika taarifa ya CIES Football Observatory ilidai kuwa nyota huyo ni MVP wa soka la dunia, ikitumia vigezo kama, umri, ubora na muda uliobaki katika mkataba ili kujua thamani ya mchezaji.

Haaland, ambaye amejifunga kuitumikia Man City hadi 2027, anaongoza katika 10 bora akiwa na thamani ya Pauni 210.8 milioni (Sh620.3 bilioni).

Kwa karibu, nyota huyo anafuatiwa na mshambuliaji wa Real Madrid raia wa Brazil, Vinicius Jr, akitajwa kuwa na thamani ya Pauni 168.9 milioni (Sh496.3 bilioni).

Pawasa awachana viongozi Simba SC
Hatma ya mkataba TPA ipo mikononi mwa Wabunge