Meneja wa Klabu Bingwa Barani Ulaya Manchester City Pep Guardiola amesema taji la kwanza la klabu hiyo la Ligi ya Mabingwa ‘limeandikwa na nyota’ na ameipongeza klabu hiyo kwa kushikamana naye wakati wengine huenda wangemfukuza kwa kuchukua muda mrefu kuwa mabingwa wa Ulaya.
Guardiola alinyanyua taji hilo mjini Istanbul nchini Uturuki Jumamosi (Juni 10) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan kwa bao la Rodri alilolifunga dakika ya 68.
“Inter ni wazuri sana. Vuta subira, nilisema wakati wa mapumziko. Lazima uwe na bahati,” Guardiola amesema.
“Iliandikwa katika nyota. Ni yetu. Kwanza kabisa maneno yangu ya kwanza ni kwa Inter, kuwapongeza kwa uchezaji wao,” amesema Guardiola akiwaambia waandishi wa habari.
“Jambo la pili ni kwa Mkurugenzi wangu wa michezo, Mkurugenzi Mtendaji na mwenyekiti wangu, kwa kawaida usiposhinda Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miaka mingi unafukuzwa.
“Moja ya sababu kubwa iliyofanya klabu hii iwe hapa tulipo ni watu kutoka Abu Dhabi. Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan alichukua klabu na bila hilo tusingekuwa hapa. Ni watu muhimu zaidi.
“Wananiunga mkono bila masharti katika kushindwa katika shindano hili. Katika klabu nyingi hilo lingetokea na wewe unafukuzwa kwa hiyo ninatoa sifa ya ajabu kwa uongozi wangu kwa Mkurugenzi Mtendaji wangu.”
Mafanikio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya pia yalikamilisha mbio tatu za City baada ya kushinda pia taji la Ligi Kuu na Kombe la FA.
Na Guardiola alifichua kwamba Jumamosi asubuhi alipokea ujumbe kutoka kwa kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson ambaye aliiwezesha klabu hiyo kutwaa mataji matatu mwaka 1999.
“Ni heshima kwangu kuwa pamoja na Sir Alex Ferguson. Lazima niseme nimepata ujumbe kwenye simu yangu ambao umenigusa sana.”
Maswali kuhusu ni lini Guardiola angeshinda tena Ligi ya Mabingwa Ulaya yalikuwa yakimfuata kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 tangu aliposhinda mara ya mwisho akiwa na Barcelona mwaka 2011.
Alikiri baada ya kuwashinda Inter ilikuwa “ahueni” kushinda tena lakini amesema sasa ana nia zaidi.