Meneja wa klabu bingwa nchinji England Manchester City Pep Guardiola ameongeza sheria katika utawala wake, kwa kuwapiga marufuku wachezaji kutumia simu wakiwa katika maeneo ya uwanja wa mazoezi.
Kwa mujibu wa gazeti la Sportsmail, meneja huyo kutoka nchini Hispania amepiga marufuku matumizi ya simu katika eneo la uwanja wa mazoezi, kwa kuamini wachezaji wengine wamekua wakipoteza muda mwingi kwa matumizi ya simu.
Guaradiola aliitambulisha sheria hiyo mpya, baada ya mazoezi ya jana Jumanne, ambapo alifanya kikao na wachezaji waliosalia kikosini katika muda huu, na kusema “Ni marufuku kutumia simu katika eneo la Gym na sehemu ya kuchezea ya uwanja wa mazoezi (City Football Academy).”
Muhanga mkubwa wa tatizo la kutumia simu katika eneo la mazoezi la Man City anatajwa kuwa Benjamin Mendy, ambaye mara kadhaa amekua akifanya hivyo kwa kuwapiga picha wachezaji wenzake, na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
Hali hiyo imekua ikimchukiza Guardiola, na mara kadhaa alimkemea lakini Mendy alionyesha kukaidi na ndipo alipoamua kuitambulisha sheria hiyo mpy,a ambayo inakwenda sambamba na adhabu ya kukatwa sehemu ya mshahara wa mchezaji atakaebainika kwenda kinyume.