Kiungo Mshambuliaji kutoka England na Klabu ya Manchester City Philip Walter Foden ataukosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi Liverpool utakaopigwa mwishoni mwa juma hili (April Mosi) baada ya kufanyiwa upasuaji wa kidole tumbo.
Foden alisherehekea ushindi wa England dhidi ya Ukraine akiwa hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji, huku klabu yake ya Man City ikipata pigo.
Kwa mujibu wa ripoti, Foden atakuwa nje ya dimba kwa muda wa wiki nne kufuatia upasuaji huo na atakosa michezo mingine ya ligi zinazofuata.
Foden alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kidole tumbo haraka iwezekanvyo kabla ya mchezo England wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Ulaya (EURO 2024) dhidi ya Ukraine, ambao England iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Lakini Foden alionekana mchangamfu baada ya upasuaji na akashahudia England ikivunja rekodi kutokana na ushindi mfululizo wa mechi za kufuzu Euro akiwa hospitali.
Foden aliwashukuru mashabiki, familia na marafiki zake kwa salamu za pole walizomtumia baada ya kufanyiwa upasuaji.
“Asanteni kwa meseji zenu, kwa sasa najisiki vizuri, naamini nitarudi haraka nikaungane na wachezaji wenzangu wa Man City,” amesema Foden 22, ambaye alifanya mazoezi na wachezaji wenzake wa England siku chache zilizopita kabla ya mechidhidi ya Ukraine.
Lakini akashindwa kuendelea na mazoezi hayo baada ya kujisikia vibaya. Pia, kiungo huyo huenda akaukosa mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Bayern Munich, michezo y Robo Fainali itachezwa kuanzia Aprili 11 na 19.