Wakati Kikosi cha Simba SC kikianza safari ya kuelekea Morocco kwa ajili ya mchezo wa wa Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca, Mshambuliaji wa klabu hiyo Moses Phiri amejipa muda zaidi wa kuendelea kufunga mabao.

Phiri anayeongoza kikosini kwa kufnga mabao (10) kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ameiangalia safu ya Ushambuliaji ambayo ndiyo eneo analocheza na kugundua kunahitajika kitu cha ziada ili Simba SC izidi kutisha zaidi akitaka kuendelea kufunga.

Mshambuliaji huyo kutoka Zambia, ambaye kasi yake ya kucheka na nyavu ilipungua alipopata majeraha Desemba mwaka jana (2022) na tangu amerejea Januari, hajawa na muendelezo mzuri, jambo ambalo alidai ni kutokana na kutopata muda wa kutosha uwanjani na mabadiliko ya timu.

Baada ya kuumia kwa Phiri, Simba SC ilimsajili Jean Baleke, ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara na hadi sasa amefunga mabao matano ya Ligi Kuu na mawili Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku michezo mingine katika eneo la Ushambuliaji akipangwa Nahodha John Bocco mwenye mabao tisa.

“Majeraha yalivuruga kila kitu. Niliporudi sikupata muda wa kutosha kujiweka sawa, ligi ilikuwa inaendelea na tayari kulikuwa na wachezaji wengine ambao walikuwa fiti zaidi, hivyo hata muda wa kucheza ili kurejesha utimamu wangu ukawa mdogo.”

“Muda huu wa mapumziko nimeutumia kujiweka sawa, sasa nipo tayari kufunga kwenye michezo nitakayopata nafasi, najiamini na najua inawezekana, hivyo mashabiki wa Simba SC waondoe shaka kwani nipo tayari kuwafurahisha zaidi,” amesema Phiri.

Kocha wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema Phiri ni mchezaji mzuri, lakini majeraha yalimpunguzia kasi ila anaamini kwa sasa amerudi kwenye ubora wake na atampa nafasi katika michezo ijayo.

“Nimekuwa nikitoa nafasi kwa wachezaji wangu, natambua ubora wa Phiri na sasa yuko timamu nadhani atapata muda mwingi wa kucheza katika michezo ijayo na atafanya vizuri,” amesema Robertinho.

Phiri alisajiliwa Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita akitokea nchini kwao Zambia akipokuwa akiitumikia Klabu ya Zanaco FC.

Kocha Yanga Princess atimuliwa
Phil Foden kuikopsa Liverpool April Mosi