Baadhi ya Wachezaji wa Simba SC wanatarajia kuondoka jijini Dar es salaam leo Jumanne (Machi 28) majira ya alasiri kuelekea Casablanca Morocco, kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Raja Casablanca.

Simba SC itacheza mchezo huo Jumamosi (April Mosi), ikiwa tayari imeshajihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali ikikusanya alama 09 katika michezo mitano iliyocheza, ikitanguliwa na wenyeji wake Raja Casablanca wanaoongoza msimamo wa Kundi C, wakiwa na alama 13.

Meneja wa Habari na Mwasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema mipango na maandalizi ya safari ya baadhi ya Wachezaji wao imeshakamilika, huku wengine walioitwa katika timu za taifa wakitarajiwa kujiunga na timu baadae.

“Kikosi chetu kinatarajiwa kuondoka Dar es salaam kuelekea Morocco saa tisa alasiri leo Jumanne kupitia Doha-Qatar, na kitafika Casablanca kesho Jumatano.”

“Msafara wetu utakuwa na wachezaji 22, lakini wanaoondoka leo ni wachezaji 13, huku wengine walioitwa kwenye timu zao za taifa wakitarajiwa kujiunga na timu moja kwa moja nchini Morocco baada ya kumaliza majukumu ya Kimataifa.” Amesema Ahmed Ally

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mwezi Februari, Simba SC ilikubali kupoteza mbele ya Raja Casablanca kwa kufungwa 3-0.

Lukaku azigonganisha klabu nguli Ulaya
Uganda yashikilia msimamo wake, yasema haipangiwi