Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limethibitisha taarifa za kusogezwa mbele kwa muda wa kuanza kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Kundi F, kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ kati ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Uganda ‘ The Cranes’.

Miamba hiyo ya Afrika Mashariki itakutana kesho Jumanne (Machi 28), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mchezo uliopita uliopigwa Uwanja wa Suez Canal nchini Misri ukishuhudia Tanzania ikichomoza na ushindi wa 0-1.

Afisa Habari na Mawasilino wa TFF Clofford Ndimbo amesema mchezo huo uliopangwa kuanza saa moja usiku, umesogezwa hadi saa mbili usiku, baada ya CAF kuridhia ombi waliloliwasilisha tangu juzi Jumamosi (Machi 25).

Ndimbo amesema sababu kubwa ya kusogezwa mbele kwa mchezo huo ni kutoa nafasi kwa watanzania wengi kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya kumaliza ibada ya kufturu katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Ushindi wa Ijumaa (Machi 24) ulikuwa wa kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi F, kwani ilianza na sare ya 1-1 na Niger ugenini kabla ya kucharazwa mabao 2-0 nyumbani na kinara, Algeria na kesho Jumanne (Machi 28) itarudiana na The Cranes ili kufufua matumaini ya kwenda AFCON 2023 kwa mara ya tatu.

Miradi umwagiliaji iboreshe hali za Wakulima: Mavunde
Nigeria: Rais mteule awashukia wapinzani, ahofia zuio kuapishwa