Bondia wa uzito wa Super Welter kutoka jijini Tanga, Hassan Mwakinyo Champez, amesema maandalizi ya pambano lake dhidi ya Kuvesa Katembo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yanaendelea vizuri, anaamini ataenda kuendeleza Rekodi yake ya ushindi nyumbani.

Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Aprili 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma katika pambano la raundi 10 lisilokuwa la ubingwa.

Pambano hilo limeandaliwa na Kampuni ya Lady in Red Promotion chini ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Sophia Mwakagenda, likilenga kukusanya taulo za kike kwa wanafunzi wa Nyanda za Juu Kusini.

Mwakinyo, amesema baada ya kukaa bila kucheza pambano katika ardhi ya nyumbani huu ni wakati wa kwenda kuwakumbusha uwepo wake na anaamini kwa maandalizi anayofanya anaenda kuibuka ushindi katika pambano hilo.

“Najua mashabiki wangu walikuwa na hamu ya kuona kile kilichotokea katika michezo iliyopita nawaahidi kuwa pambano hili litakuwa la aina yake narudi ulingoni baada ya kupoteza lakini nawaahidi watarajie mchezo mzuri siku hiyo,” amesema Mwakinyo.

Mara ya mwisho Mwakinyo kucheza pambano hapa nchini ilikuwa Septemba 3, 2021 aliposhinda kwa TKO.

Mo Farah kukiwasha Port-Gentil Marathon
Siri ya ushindi wa Karim Mandonga yafichuka