Siku chache kabla ya kuivaa TP Mazembe katika mchezo wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Kocha Mkuu wa young Africans Nasreddine Nabi amesema bado wana kibarua kigumu kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano hiyo.

Young Africans itakuwa ugenini Aprili 02 mwaka huu, katika mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe huku ikiwa na Rekodi ya kuifunga mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Nabi amesema wana kibarua kigumu katika mshindano hayo, hivyo hataki kuona wachezaji wake wakibweteka ili kuhakikisha wanatimiza malengo waliojiwekea msimu huu kwa kupambana katika kila mchezo.

“Sitaki kuona mchezaji wangu yeyote akibweteka baada ya kufuzu robo fainali kwani bado tuna kibarua kigumu cha kuhakikisha tunafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa pamoja na michezo yetu ya Ligi Kuu,” amesema Nabi.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema kuwa anataka kuona mchezo wao wa mwisho dhidi ya TP Mazembe wanapata ushindi ili kumaliza hatua ya Makundi wakiwa kileleni mwa msimamo wa Kundi D.

Amesema anajua mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa kutokana na kwenda kucheza ugenini.

Young Africans ilitinga hatua ya Robo Fainali baada ya kuifunga US Monastir mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Jumapili (Machi 19), Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walianza michuano hiyo kwa kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ha Us Monastir, ikawacharaza TP Mazembe mabao 3-1, ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako, ikaifunga mabao AS Real Bamako mabao 2-0 kabla ya kuifunga US Monastir mabao 2-0.

Katika msimamo wa kundi D Young Africans ipo kileleni kwa alama 10 sawa na US Monastir wakifuatiwa na AS Real Bamako akiwa na alama 05 na TP Mazembe ikiwa na alama 03, ambapo Young Africans na US Monastir tayari zimeshafuzu hatua ya Robo Fainali.

Siri ya ushindi wa Karim Mandonga yafichuka
Ilkay Gundogan amnyima usingizi Xavi