Mwanariadha kutoka England Mo Farah atashiriki mbio za kilometa 10 za Port-Gentil nchini Gabon majuma mawili kabla ya gwiji huyo kushiriki mbio zake za mwisho jijini London.

Farah mwenye medali za Olimpiki za mbio za meta 5,000 na 10,000, atashiriki London Marathon kabla ya kustaafu rasmi kucheza mchezo huo.

Bingwa huyo mara nne wa Olimpiki, mwenye umri wa miaka 40, Januari alitangaza kuwa huu ni mwaka wake wa mwisho kukimbia kabla kustaafu rasmi.

Farah kwa sasa anajifua nchini Ethiopia wakati akiendelea kujiandaa kwa ajili ya London Marathon itakayofanyika Aprili 23, 2023.

Hata hivyo, hana uhakika kama marathoni hiyo ndio itakuwa shindano lake la mwisho la kiushindani.

Katika video fupi, mwanariadha huyo anayeshikilia rekodi ya marathoni Uingereza amesema “anajiandaa vizuri  nchini Ethiopia, yuko vizuri na yuko tayari kujaribu katika mbio za kilometa 10 Aprili 8 Gabon,” siku 15 kabla hajashuka katika mitaa ya jijini kwake na kushindana.

Maumivu ya paja yalimzuia Farah kushiriki katika London Marathon ya mwaka jana, huku mbio za mwaka 2023 zikionekana kuwa za kwanza za Marathoni kamili tangu mwaka 2019.

Bingwa huyo mara sita wa uwanjani alishinda mbio za ‘Big Half’ jijini London Septemba lakini amekimbia mara saba tu tangu Oktoba mwaka 2019.

Muda bora na binafsi wa Farah katika mbio za kilometa 10 barabarani ni dakika 27:44, hata hivyo, muda huo aliuweka mwaka 2010 na alishangazwa baada ya kupitwa na mkimbiaji wa klabu yao Ellis Cross katika mbio za mwisho za umbali huo jijini hapa mwaka jana katika mita 10,000.

Mshindi wa mwaka 2018 wa Chicago Marathon huku mshindi wa London Marathon alimaliza wa tatu mwaka 2018. Atashiriki katika mbio za mwaka 2023, ambazo zitashirikisha nyota wanne kati ya watano wenye kasi zaidi duniani.

Nigeria: Rais mteule awashukia wapinzani, ahofia zuio kuapishwa
Mwakinyo aahidi kumchapa Kuvesa Katembo