Mwimbaji kutoka Canada, Justin Bieber ameweka rekodi nyingine kwenye mtandao wa Twitter baada ya kufikisha wafuasi (followers) milioni 100.
Bieber ameweka rekodi hiyo na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye mtandao huo kama mtu mwenye wafuasi wengi zaidi, akimfuatia Katy Perry ambaye anamzidi takribani wafuasi milioni 3.
Kwa rekodi hiyo, Bieber amempita Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama ambaye anashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa Twitter akiwa na wafuasi milioni 94.
Aidha, Bieber anaonekana kutengeneza himaya nyingine kubwa zaidi kwenye mtandao wa Instagram akiikaribia idadi ya milioni 100 kwani hadi sasa anawafuasi milioni 91 na laki tano.
Hata hivyo, kwenye mtandao huo Bieber anashika nafasi ya kumi huku nafasi ya pili ikishikiliwa na aliyekuwa mpenzi wake, Selena Gomez akiwa na wafuasi milioni 124. Selena anaifuatia akaunti ya mtandao wa Instagram ambayo inashika nafasi ya kwanza ikiwa na wafuasi milioni 225.
- Azam FC kupimana na ‘Trans Camp’ leo Chamazi
- Mwakyembe apinga vikali uzushi juu ya ubovu wa ndege za Bombardier
Saa chache zilizopita, msanii huyo amemulikwa na kamera za paparazi muda mfupi baada ya kuweka rekodi hiyo akiwa na kitabu cha dini akielekea kwenye ibada ikiwa ni sehemu ya ratiba yake mpya tangu atangaze kumrudia Mungu na kuachana na mambo ya dunia yaliyo kinyume na mafundisho ya dini.
Katika safari hiyo ya kuelekea kanisani, Bieber aliongozana na mtoto wa muigizaji maarufu, Arnold Schwarzenegger.