Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara leo asubuhi kimerejea jijini Dar es salaam kikitokea Musoma, Mara kilipokwenda kucheza mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United Mara.
Baada ya ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya wenyeji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, kikosi cha Simba SC kilianza safari jana jioni kutoka Musoma, Mara kuelekea Mwanza na leo asubuhi kilipanda ndege kurejea Dar es salaam.
Simba SC imelazimika kurejea haraka jijini humo, kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri.
Simba SC ilianza vyema michuano hiyo ya Afrika kwa kuifunga AS Vita Club 1-0 mwishoni mwa juma lililopita mjini Kinshasa, DR Congo, huku Al Ahly wakiigunga El Mereikh ya Sudan 3-0.
Mchezo wa Simba SC dhidi ya Al Ahly utachezwa Jumanne (Februari 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.