Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Innocent Bashungwa, Jana Jumatano (Februari 03) alifanya ziara kwenye makao makuu ya Azam FC, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mh. Bashungwa aliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Mh. Yusuph Singo, alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujionea kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC (Azam Academy) sambamba na miundombinu iliyopo ndani ya Azam Complex.
Waziri huyo alipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ na Maofisa wengine wa timu hiyo, akipata nafasi ya kutembelea mabweni ya wachezaji na miundombinu yote mingine iliyopo katika viunga vya Azam Complex.
Bashungwa, alifurahishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Azam FC, akidai ni faida kubwa kwa Taifa huku akiahidi wao kama serikali wataendelea kuunga mkono jitihada hizo zinazofanywa na timu hiyo.