Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kimeanza safari ya kuelekea Mkoani Morogoro tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 19 wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa keshokutwa Jumamosi (Desemba 31) katika Uwanja wa Manungu Complex, Wilayani Mvomero mkoani Morogoro, kuanzia mishale ya saa kumi jioni.
Young Africans imeanza safari majira ya mchana, baada ya mapema leo Alhamis (Desemba 29) asubuhi, kufanya mazoezi ya mwisho kambini kwao Avic Town Kigamboni, jijini Dar es salaam.
Mabingwa hao wanaelekea Morogoro wakiwa bado kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumiliki alama 47, wakifuatiwa na Watani zao wa Jadi Simba SC wenye alama 41, huku Azam FC akisalia nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 37.
Mtibwa Sugar watakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuondoa dhamira ya kuendelea kupoteza katika Michezo ya Ligi Kuu, kwani mara ya mwisho walipoteza mchezo wao dhidi ya Ihefu FC kwa kufungwa 3-1.
Mtibwa Sugar inayohitaji ushindi dhidi ya Young Africans inashika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 24, baada ya kucheza michezo 18 ikishinda sita, ikipoteza sita na sare sita.