Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda amewaasa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaotarajia kustaafu hivi karibuni kudumisha nidhamu katika matumizi ya fedha baada ya kustaafu utumishi wa umma na kujikita katika shughuli za uzalishaji.
Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati watumishi hao walipomtembelea katika makazi yake yaliyopo Zuzu kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji katika sekta ya kilimo na mifugo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kustaafu pamoja na kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma.
Amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa watumishi wote wanaotarajia kustaafu kujenga utamaduni wa nidhamu katika matumizi ya rasilimali ikiwemo fedha watakazopata kama kiinua mgongo.
” Nidhamu ya maisha baada ya kustaafu ni muhimu sana hivyo niwaase mjitahidi kuacha baadhi ya masuala ambayo mnafanya kwasasa kama starehe na mambo yote yanayoendana na kupoteza muda wenu badala yake mjikite katika uzalishaji,” amesema Pinda
Aidha, amesema kuwa ni vyema watumishi hao wakajenga utamaduni wa kufanya kazi za uzalishaji na kujikita katika usimamizi wa miradi ya uzalishaji watakayoanzisha kwa lengo la kujiongezea kipato na kukuza uchumi .
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Maimuna Tarishi amesema kuwa mafunzo yakuwajengea uwezo wa kujiandaa kustaafu, yameandaliwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.
Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mafunzo ya siku 5 kwa watumishi wake wanaotarajia kustaafu ili kuwapa mbinu za kisasa zinazolenga kuwawezesha kuendelea na maisha yao baada ya kustaafu huku wakiendeleza shughuli za uzalishaji zitakazowawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku na kuweza kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya kustaafu.