Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Barani Ulaya *UEFA* Michel Platini anashukiwa kushiriki kufanya uhalifu katika malipo ya dola milioni 2 kutoka Shirikisho la Soka Duniani *FIFA*.
Platini ambaye pia aliwahi kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kama nahodha ameanza kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo, ambazo zinaendelea kumchafua katika ramani ya soka duniani.
Muendesha mashitaka wa Uswisi asubuhi leo alianza kumuhoji gwiji huyo wa soka, juu ya malipo ya dola milioni 2 aliyopokea kutoka FIFA mwaka 2011.
Platini rasmi ni mshukiwa wa malipo hayo ambayo yalipelekea kuondolewa kwake madarakani kama Rais wa UEFA, pia alienguliwa kwenye mchakato wa kuwania kiti cha urais wa FIFA, ambapo wachunguzi wa Serikali kuu ya Uswisi walifichua madai hayo miaka mitano iliyopita.
Platini mwenye umri wa miaka 65 anashukiwa kuwa mshirika wa uhalifu wa ubadhirifu, wa matumizi mabaya ya fedha na kitendo cha kughushi, kwa mujibu wa nyaraka zilizothibitishwa na shirika la habari la Associated Press mwezi Juni.