Kocha mkuu wa klabu ya Tottenham Hotspur ya nchini England, Mauricio Pochettino, amesema matumizi ya teknolojia ya uamuzi kwa kutumia video inayofahamika kama ‘Video Assistance Referee’ (VAR) kutatua utata unaojitokeza kwenye mchezo wa mpira wa miguu inaua mchezo wa soka.
Pochettino ametoa kauli hiyo baada ya kukataliwa magoli mawili waliyofunga katika mchezo wa Kombe la FA waliokuwa wanacheza dhidi Rochdale, licha ya kupata ushindi wa mabao 6-1 na kutinga robo fainali.
Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Wembley uligubikwa na matukio ya utata ambapo mara kadhaa mwamuzi alionekana kwenda kutazama video ili kufanya uamuzi ambao haukuwa ukiuridhisha upande wa Tottenham.
“Nina furaha kwa sababu kazi nimemaliza na tumeingia robo fainali, lakini sina uhakika kwamba mfumo wa video assistance referee utatusaidia. Nadhani mpira wa miguu, ni muktadha wa hisia, kama tunaenda kuua hisia za mpira, nadhani mashabiki na watu wenye upendo na soka hawakuwa na furaha kwa walichokiona leo,” amesema Pochettino baada ya mchezo huo.