Afisa wa polisi nchini Tunisia amewauwa watu wanne katika sinagogi kongwe zaidi barani Afrika, katika shambulio lililoibua hamaki wakati wa hijja ya kila mwaka ya Mayahudi kwenye kisiwa cha Djerba.
Wizara ya mambo ya ndani nchini humo, imesema askari huyo aliwapiga risasi wageni wawili, akiwemo raia wa Ufaransa, na askari wenzake wawili, kabla ya yeye mwenyewe kupigwa risasi na kuuawa.
Wageni wengine wanne na maafisa wa watato wa polisi walijeruhiwa katika shambulio hilo, la kwanza dhidi ya wageni kutoka nje nchini Tunisia tangu 2015, na la kwanza dhidi ya mahujjaji wa Sinagogi la Ghriba tangu shambulio la kujitoa muhanga lililoua watu 21 mwaka 2002.
Wizara ya mambo ya nje ya Tunisia iliwatambua wageni wawili waliouawa kuwa ni raia wa Tunisia mwenye umri wa miaka 30 na raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 42, lakini haikutoa majina yao.