Sakata la kesi ya uchochezi linalomkabiri Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu lililopelekea Chama hicho cha wanasheria kulaani kitendo hicho na kutaka aachiliwe, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lucas Mkondya amesema kuwa kamwe hawatamwachia kwa sasa mpaka pale upelelezi utakapokamilika.
Amesema kuwa polisi haitoi dhamana kwa Lissu bali mahakama ndiyo itakayofanya hivyo baada ya jeshi hilo kukamilisha uchunguzi wake na kumfikisha katika chombo hicho ili taratibu zingine zifuate.
“Tukimaliza upelelezi wetu ndipo tutakapomfikisha mahakamani, lakini kwasasa bado tunaendelea na upelelezi wetu na hatujajua tutamaliza lini, lakini tutakapokamilisha tutamfikisha kwenye chombo husika,”amesema Mkondya.
Hata hivyo, Chama cha Wanasheria Tanganyika TLS kimelitaka Jeshi hilo la Polisi kutoa dhamana kwa Lissu kwa sababu ni haki yake kikatiba na kosa alilotuhumiwa nalo linadhaminika kisheria au kumfikisha mahakamani ili apate haki yake.