Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 683 wa makosa mbalimbali katika oparesheni iliyochukua wiki tatu katika wilaya zote za mkoa huo.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Oparesheni Maalum za Jeshi la Polisi Tanzania Kamishna Mwandamizi wa Jeshi la Polisi SACP Mihayo Msikela wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora kuhusiana na oparesheni hiyo.
Mihayo amesema miongoni mwa watuhumiwa hao ni 277 wamefikishwa mahakamani na kuhukumiwa , watuhumiwa 255 bado kesi zao zinaendelea na watuhumiwa 42 wako katika uangalizi wa polisi baada ya kutokuwepo kwa ushahidi madhubuti.
Baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa ni silaha aina ya gobole moja, mapanga tisa, meno ya tembo mawili, pikipiki 34 , magodoro 10, simu za mkononi nne, vyuma vya reli viwili, runinga za aina mbalimbali 19, mfano wa sare za majeshi mbalimbali ya ndani na nje na pombe haramu ya gongo lita 408.
Aidha, katika operesheni hiyo iliyoanza Desemba 7 mwaka huu, jeshi la polisi limebaini kuwa magenge yanayojihusisha na uvunjaji wa nyumba, uporaji na wizi ni vijana ambao umri wao ni kuanzia miaka 15 hadi 21, na kusema litaendelea kufanya oparesheni na misako ya mara kwa mara.